Na Julius Konala
HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma ipo hatarini
kukumbwa na baa la njaa kutokana na baadhi ya wakulima kuanza kuvuna mahindi
mabichi yakiwa shambani na kuyauza.
Aidha tulipita maeneo mbalimbali ya masoko ya uuzaji wa
mazao ya mahindi likiwamo soko kubwa la Sodeco lililopo katika Halmashauri ya
Manispaa ya Songea mkoani humo na kushuhudia hali hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya
wafanyabiashara walisema hali hiyo inatokana na serikali ya mkoa kushindwa
kutoa vibali vya kununulia mahindi ya mwaka jana katika ghala la hifadhi ya
chakula la taifa.
Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara ambaye pia ni
Mkurugenzi wa kampuni ya kukoboa na kusaga nafaka ya Mtanzamo, Julius Mlawa,
alisema lengo la serikali ya Mkoa wa Ruvuma kutaka kutoa vibali vya kununua
mahindi kwenye ghala la chakula la taifa kwa kipindi kile lilikuwa zuri, lakini
kwa sasa mpango huo hautafanikiwa kutokana na serikali kutaka bei ya sh 450 kwa
kilo moja wakati sasa wakulima wanauza sh 300 kwa kilo.
Alisema kwa ujumla wafanyabiashara mara zote wamekuwa
wakisukumwa na soko lililopo, kwani wakulima walishaanza kuuza mahindi mapya
tofauti na kipindi cha nyuma ambacho Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu,
alipoahidi kutoa vibali vya kununua mahindi kutoka hifadhi ya chakula ya taifa
ambapo mahindi mapya yalikuwa bado hayajaanza kuvunwa.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Mkirikiti, amepiga marufuku
kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa mahindi mabichi kutoka kwa
wakulima na kusema kufanya hivyo ni kuwanyonya wakulima na kukaribisha janga la
njaa na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mfanyabiashara
yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
EmoticonEmoticon