Na Frank Joachim
Taarifa Kwa Umma
Kitendo cha kulifungia gazeti la
MwanaHalisi kwa muda usiojulikana kinaweza kusababisha hofu kubwa kwa watetezi
wa haki za binadamu na wanahabari kwa ujumla. Kitendo hicho kinafuatia kile cha
kuwakamata na kuwaweka rumande (Oysterbay Polisi) wanaharakati zaidi ya kumi
kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kuandamana kufuatia mgomo wa Madaktari mnamo
tarehe 9 mwezi Februari 2012.
MISA –Tanzania inalaani vikali
matumizi mabaya ya Dola katika kunyamazisha wanahabari wanapojaribu na
kuthubutu kufuatilia matukio mbalimbali na kuarifu umma kuhusu yale
waliyoyafanyia kazi kwa kina. Ni rai yetu kwa serikali kuwa ni vyema wabainishe
taarifa mahsusi zilizopelekea maamuzi ya kufungia gazeti la MwanaHalisi ili
kutuondolea hofu sisi tunaotetea haki na uhuru wa vyombo vya habari. Kuendelea
kuficha taarifa husika ni kuendelea kuikanyaga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977 (ibara ya 18) kupitia kivuli cha Sheria ya Magazeti ya mwaka
1976 ambayo kimsingi imepitwa na wakati na haiwezi kutumika kinyume na Katiba
ya nchi.
Ni rai yetu pia kwa serikali ya
Tanzania kwamba izingatie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika yale
yenye kuhamasisha utoaji haki kuliko kujikita kwenye kifungu cha 30 cha Katiba
hiyo ambacho kimsingi kinaweka mipaka maalumu ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mipaka hiyo haionekani kuzingatiwa na serikali katika kulifungia gazeti la
MwanaHalisi.
Kwa taarifa hii kwa umma,
tunaiomba pia serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulifungulia gazeti
la MwanaHalisi mapema iwezekanavyo na bila masharti ili kuwawezesha watanzania
kuendelea kunufaika na taarifa zinazochapishwa na gazeti hilo ilmradi maadili
ya uandishi wa habari yazingatiwe.
Hii ni haki ya msingi kwa kila mtu na ni
vyema aione ikitekelezeka.
Taarifa hii imetolewa na kusaini
hapa Dar es salaam leo tarehe 31 Julai 2012.
Mohammed Tibanyendera
Mwenyekiti, MISA-TAN
EmoticonEmoticon