DAR ES SALAAM, Tanzania
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imeiamuru Benki ya
Standard Chartered ya Hong Kong (SCBHK) na Shirika la Usambazaji Umeme
Tanzania (Tanesco) kuacha kuingilia utulivu, umiliki, usimamizi na utawala wa
mitambo ya ufuaji umeme ya Harbinder Singh Sethi iliyopo Tegeta, na kusubiri
uamuzi wa mwisho wa kesi ya msingi.
Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL) na Pan African Power Solutions Limited (PAP) zilifungua kesi kwa kuhoji
uhalali wa maamuzi ya Kituo cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya Uwekezaji
(ICSID) dhidi ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) na Martha
Renju (anayedaiwa kuwa msimamizi wa mali zake), iliyotolewa katika kesi ya ICSD
namba ARB / 10/20.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Dk. Fauz
Twaib na kusomwa kwa niaba yake na Jaji Amri Msumi Hamisi, Jaji Twaib aliamuru
Tanesco kutofanya biashara yoyote na SCB-HK au Martha Renju kwa niaba ya IPTL /
PAP bila ya idhini ya kimaandishi kutoka IPTL / PAP.
“Wadaiwa kwa pamoja wanazuiliwa kufanya
utekelezaji wa maamuzi iliyotolewa katika chombo cha kimataifa ya ICSD yenye
namba ARB / 10/20 na kusambazwa kwa wahusika Februari 12, 2014, kwa namna yoyote
ile, na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya mdai, ” ilisomeka sehemu ya
hukumu hiyo.
Tanesco pia imezuiwa kutolipa kwa SCB-HK na
Martha Renju malipo yoyote wanayostahili IPTL / PAP bila ya idhini ya maandishi
kutoka kwa IPTL / PAP.
Mahakama pia imeizuia Tanesco kutotekeleza au
kukubaliana na au kuyatekeleza maamuzi ya ICSID, na kusubiri uamuzi wa mwisho
wa kesi yao ya msingi.
Pia mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja ya
mwanasheria wa SCB-HK, Charles Morrison, ambaye alisema Mahakama Kuu ya Tanzania
haipaswi kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya ombi hilo sababu Tanzania ni
mwanachama wa ICSID ambayo pia inajulikana kama Washington Convention au ICSID
.
Kwa mujibu wa Jaji Twaib, Wakili Morrison
alionya kuwa kama Tanzania haitotii wajibu huo, itajiweka sehemu mbaya katika
nyanja ya kimataifa.
EmoticonEmoticon