NASRA ABDALLAH, Dar Es Salaam, Tanzania
RAIS Jakaya Kikwete, amesema kuanzia Juni
mwakani kila kinachofanyika katika jiji la Dar es Salaam kinaonekana katika
mitambo itakayokuwapo kila mahali.
Alisema kutokana na kufungwa kwa mitambo hiyo
waharibifu wa miundombinu, vibaka na wahalifu hawatoweza kufisha matendo yao.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana Jijini Dar
es Salaam wakati wa hafla ya kufungua barabara ya Tegeta – Mwenge iliyojengwa
kwa kiwango cha lami huku ikiwa na urefu wa kilometa 12.9.
Alisema inasikitisha kuona serikali ikiingia
gharama kubwa katika kutengeneza barabara halafu watu wasiokuwa na uchungu na
fedha hizo za walipa kodi wakiharibu miundombinu hiyo kwa maslahi ya matumbo
yao.
“Tumeshaongea vya kutosha jamani katika hili
sasa dawa ya watu wa aina hii ipo jikoni na Juni mwakani watu wote hawa
tutawakamata kirahisi tu hawatakuwa na pa kukimbilia,”alisema.
Hata hivyo Rais Kikwete, hakuwa tayari kueleza
ni mitambo ya aina gani itakayofungwa lakini katika nchi mbalimbali kumekuwa na
kamera katika mitaa ambazo zinarekodi kila kinachofanyika.
Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara ya
Tegeta-Mwenge, itasaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es
Salaam na hii ni baada ya kukaribia kumalizika kwa barabara ya Msata Bagamoyo.
Alisema kutokana na tatizo la foleni lililopo
katika Jiji hilo, ambapo hata mihadi ya watu kukutana siku hizi imekuwa ni
taabu, Serikali imekuwa ikijitahidi kutafuta njia mbalimbali za kutatua kero
hiyo ikiwemo kuboresha vyombo vya usafiri wa umma na utengenezaji wa barabara
za mchepuko.
Hata hivyo aliwataka wananchi kujua kuwa tatizo
la foleni halipo tu Dar es Salaam bali hata kwanye nchi zilizoendelea ikiwemo
Newyork Marekani na China.
Rais Kikwete, alisema hii inachangiwa na kukua
kwa maendeleo ambapo kwa Tanzania mwaka 1980 magari yaliyokuwa yakipita
barabarani ni yale ya Serikali na kwa watu binafsi ilikuwa lazima uombe kibali
kabla ya kununua gari.
“Lakini hivi sasa familia nyingi zinamiliki
magari na nyingine zimeenda mbali zaidi ambapo baba ana gari lake, mama na
watoto na bado watu wataendelea kumiliki magari siku za baadaye yote hii
imechangiwa na kubadilika kwa mfumo wa maisha na nchi kupiga hatua ya maendeleo
kwa watu wake,”alisema.
Alisema ameziagiza Mamlaka husika kuboresha
usafiri wa reli kwa kuongeza njia za reli katika maeneo mbalimbali ya Jiji la
Dar es Salaam na kuleta mabehewa yatakayoendana mahitaji.
Alisema pia serikali ipo mbioni kuanzisha kivuko
kitakachotoa huduma kwa wakazi wa Bagamoyo na Tegeta na kujenga miji mingine
nje ya mji ili huduma zinazofuatwa mjini zipatikane huko huko walipo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Alhaj
Mussa Iyombe, alisema barabara hiyo imetengenezwa kwa msaada mkubwa wa Serikali
ya Japan ambako shilingi bilioni 99.6 zimetumika kukamilisha mradi huo.
Naye Balozi wa Japan hapa nchini, Masaki Okada,
alisema Serikali yake inaamini kuwa barabara ni kichocheo kikubwa katika ukuaji
wa uchumi na kipaumbele chake cha kwanza ni ujenzi wa barabara.
EmoticonEmoticon