TANZANIA DAIMA, Arusha
JESHI la polisi Mkoa wa Arusha
limemuua kwa kumpiga risasi mtuhumiwa wa ugaidi, Yahaya Hassan Omari Hela (31)
‘Yahaya Sensei’ mkazi wa Mianzini mjini hapa.
Mtuhumiwa huyo alipigwa risasi ya
mguu na kalio la kulia eneo ya Kisongo wilayani Monduli alijaribu kuruka kwenye
gari la polisi kwa lengo la kuwatoroka.
Kamanda wa polisi mkoani hapa,
Liberatus Sabas aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa tukio
hilo lilitokea Oktoba 19 mwaka huu saa 5 usiku wakielekea kijiji cha Chemchem
wilayani Kondoa, Dodoma alikozaliwa mtuhumiwa huyo ili akawaoneshe alipohifadhi
mabomu.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye
alikuwa mwalimu wa Karate na Judo alikuwa muasisi na kinara wa matukio ya
ugaidi yaliojitokeza Jijini Arusha, Zanzibar, Mwanza na Dar es Salaam.
Kamanda Sabas, alisema walifanikiwa
kumkamata baada ya kumtafuta muda mrefu kwa kutumia intelijensia ya polisi ya
kisasa na hali ya juu kabla ya kumkamata mkoani Morogoro Oktoba 6 na kupelekwa
Arusha Oktoba 11.
Alisema mtuhumiwa huyo alipohojiwa
alikiri kuratibu matukio mbalimbali ya ugaidi.
Baada ya kupigwa risasi hizo
alifariki dunia akiwa njiani kuwahishwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru
kwa matibabu na kwamba mwili wake katika hospitali hiyo.
Sabas aliyataja baadhi ya matukio
mtuhumiwa huyo aliyokiri kuhusika kuwa ni lile la Oktoba 25, 2012 saa 5:30
usiku katika mtaa wa Kanisani Paloti kata ya Sokoini One jijini hapa ambapo
yeye na wenzake walitega bomu nyumbani kwa Abdulkarim Idd Jonjo (52) katika
chumba alicholala na kumjeruhi.
Kamanda Sabas alisema mtuhumiwa huyo
alikiri kushiriki tukio la Mei 5 mwaka 2013 saa 10:30 eneo la Kanisa la
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo Olasiti jijini Arusha ambapo
aliratibu kurushwa kwa bomu na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 56.
Tukio la tatu lilitokea Juni 15
mwaka 2013 saa 11:50 jioni katika Viwanja vya Soweto Kata ya Kaloleni Jijini
Arusha, ambapo marehemu na wenzake walirusha bomu na kujeruhi watu 60 na wanne
kufariki dunia waliokuwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kamanda Sabas Alitaja matukio mengine
aliyokiri kuhusika nayo ni lile la Julai 11 mwaka 2013 eneo la kwa Mrombo
jijini hapa, ambapo alishirikiana na wenzake kumwagia tindikali usoni Sheikh
Said Juma Makamba.
Tukio jingine ni lile la Februari 12
mwaka 2014 saa eneo la Tindigani Unga limited jijini hapa kwenye msikiti wa
Sawiyatu Qadiria, walipommwagia tindikali usoni Sheikh Hassan Bashir.
Tukio la sita la Februari 28 mwaka
2014 saa 5:15 alfajiri huko msikiti wa Bondeni Jijini Arusha, marehemu na
wenzake walimwagia tindikali Mistapha Mohamed Kiago na kumjeruhi usoni na
shingoni.
Tukio la saba Aprili 13 mwaka 2014
saa 1:30 usiku, eneo la Mianzini, huko nyumba ya kulala wageni na Baa ya Night
Park, walirusha bomu na kujeruhi watu kumi na mtu mmoja kusababisha kifo chake.
Kamanda alitaja tukio lingine
aliloshiriki ni la Aprili 13 mwaka 2014 la saa 5 eneo la Majengo jijini Arusha,
alirusha bomu kwa kushirikina na wenzake na kujeruhi watu wawili Sudi Ali Sudi
(37) ambaye ni Mkurugenzi wa Answar Muslim kanda ya Kaskazini na mwenzake
Muhaji Hussein Kifea (38) mkazi wa Dare s Salaam.
Tukio la tisa mtuhumiwa huyo
anadaiwa kuwa Julai 7 mwaka 2014 saa 4:15 usiku eneo la uzunguni, mgahawa wa
vama Traditional Indian uliopo jirani na Viwanja vya Gymkhana alirusha bomu na
kujeruhi watu nane.
EmoticonEmoticon