Na Edwin Moshi
MAKETE
Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Makete wametakiwa kutoa
ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi la sensa ya watu na Makazi wilayani
hapo linalotarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu
Akifungua mafunzo yahusuyo sensa kwa madiwani wa halmashauri
hiyo mwishoni mwa wiki, mgeni rasmi katika mafunzo hayo Mkuu wa wilaya ya
Makete Josephine Matiro amesema madiwani hao wana nafasi kubwa ya kuisaidia
serikali kukamilisha zoezi hilo kwa kuwaelimisha wananchi waliopo kwenye kata
zao
Pia Matiro ameongeza kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi
halitaathiri shughuli za wananchi za kujipatia kipato hivyo kuwataka madiwani
hao kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa zoezi hilo
“Waheshimiwa madiwani serikali inatambua nguvu mliyonayo kwa
wananchi mnao waongoza, tunategemea ushirikiano wenu pindi mnapokutana na
wananchi huko, tafadhalini sana mtusaidie kuielimisha jamii kuhusu suala la
sensa ya watu na makazi itakayofanyika siku chache zijazo” alisema Matiro
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Geofrey Masaki
amesema serikali imelipa kipaumbele zoezi la sensa ya watu na makazi na ndio
maana imeweza kutoa mafunzo kwa makarani wote watakao husika na utekelezaji wa
zoezi hilo , na hata kwa wadau mbalimbali wakiwemo madiwani
Amesema wasisite kuielimisha jamii kushiriki katika zoezi
hilo , na kutaka zoezi la sensa kutohusishwa kisiasa
Akizungumza mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo diwani wa
kata ya Iniho ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa halamshauri ya wilaya ya
Makete Mh. Jison Mbalizi, amesema anaamini yeye pamoja na madiwani wenzake
wataielimisha jamii kuhusu umuhimu wa sensa na pia hawatarajii kuhusisha suala
la sensa na siasa kama inavyodhaniwa na watu wengi
Pia alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuondokana na
dhana potofu kuwa sensa haina umuhimu wowote na kuwataka wananchi hao kushiriki
bila woga
Sensa ya watu na makazi itafanyika usiku wa Agosti 25
kuamkia Agosti 26 ikiwa na kauli mbiu isemayo sensa kwa maendeleo jiandae
kuhesabiwa
EmoticonEmoticon