Papa Benedicto XVI |
Baba Mtakatifu Benedikto wa 16 amerejea wito wake kwa Jumuiya ya Kimataifa, wa kumaliza machafuko nchini Syria, huku akiyataka mataifa makubwa kutosita katika juhudi za kumaliza mgogoro huo. Baada ya kutoa baraka kwa waumini wake huko Castel Gandolfo, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema anafuatilia kwa karibu ghasia hizo na ameziomba nchi jirani kuwapokea wakimbizi na kuwapa msaada wote wanaouhitaji. Ameshauri njia ya majadiliano itumike ili kufikia suluhisho la kisiasa kwa amani. Na taarifa kutoka Jordan, zinasema kuwa serikali hiyo imefungua kambi yake ya kwanza kwa maelfu ya wakimbizi wanaokimbia ghasia nchini Syria. Kambi hiyo ya Zaatari iliyojengwa kwa maturubali iko jangwani, jirani na mji wa Mafraq na ina uwezo wa kuwahifadhi wakimbizi 120,000. Baada ya kuzinduliwa kwa kambi hiyo na serikali ya Jordan na Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje, Nasser Judeh amesema hatua hiyo ni sehemu ya msaada wa nchi yake kwa Wasyria hao wasio na makazi, ambao wanaingia Jordan kwa makisio ya watu 2,000 kwa siku.
EmoticonEmoticon