Habari kutoka Nigeria zinasema kuwa, watu
wanaoaminika kuwa wanamgambo wa Boko Haram wamewateka nyara wasichana 8 katika
kijiji cha Warabe kilichoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Habari zaidi
zinasema kuwa, wasichana hao wenye umri wa kati ya miaka 12 na 15 walitekwa
nyara wakati watu hao wenye silaha walipovamia kijiji hicho na kupora mifugo
pamoja na vyakula. Tukio hilo limejiri siku moja baada ya Boko Haram kutangaza
kwamba linawashikilia zaidi ya yanafunzi wa kike 200 waliotekwa nyara katika
shule moja mjini Chibok mwezi uliopita. Kiongozi wa Boko Haram,
Abubakar Shekau
ametishia kuwauza wasichana hao ndani na nje ya Nigeria.
Umoja wa Mataifa umeonya kundi la Boko Haram
ukisema kuwauza wanafunzi hao wa kike ni kinyume cha sheria za kimataifa
zinazopinga biashara ya utumwa na hatua hiyo itapelekea wanachama wa kundi hilo
kutafutwa kwa kosa la kutenda jinai dhidi ya binadamu.
Siku ya Jumapili Rais Goodluck Jonathan alisema
serikali yake inafanya juhudi zote kuwatafuta na kuwaokoa wasichana hao na
akaziomba baadhi ya nchi za Magharibi kuisaidia serikali yake katika suala
hilo.
EmoticonEmoticon