Na Fidelis Butahe na Habel
Chidawali ,Dar/Dodoma.
Wakati
Katiba inayopendekezwa ikikabidhiwa kesho kwa Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti
wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema hata
akialikwa katika sherehe hizo hatahudhuria kutokana na majukumu aliyonayo kwa
sasa.
Jaji Warioba alisema angependa
kuhudhuria sherehe hiyo ambayo pia itahudhuriwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, wakuu wa mikoa, mabalozi na wageni mbalimbali, lakini kutokana na
dharura aliyoipata haitawezekana.
Sherehe hiyo itafanyika mkoani
Dodoma kesho na Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta
atakabidhi nakala ya Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Katika hafla hiyo itakayofanyika
kwenye Uwanja wa Jamhuri, wajumbe wa Bunge hilo walioshiriki mchakato huo
kuanzia mwanzo mpaka mwisho watapewa vyeti.
Akizungumza na gazeti hili jana,
Jaji Warioba alisema hadi jana hakuwa amepata mwaliko lakini hata kama akipewa
hataweza kuhudhuria. “Siwezi kutoka nje ya Dar es Salaam kwa siku mbili tatu
hizi kwa sababu nina dharura. Kama wakinialika nitawaomba radhi kwamba sitaweza
kuhudhuria,” alisema.
Alipoulizwa iwapo Jaji Warioba ni
miongoni mwa waalikwa katika sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema
Nchimbi alisema angetoa majibu leo kuhusu suala hilo lakini anaamini mkongwe
huyo ni miongoni mwa viongozi wastaafu, hivyo kualikwa ni lazima.
Sherehe yenyewe
Mkuu huyo wa mkoa alisema sherehe
hizo zitatanguliwa na dua ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza Bunge hilo salama
ambayo itafanyika leo mchana katika Bustani ya Mwalimu Nyerere.
Wageni wengine walioalikwa ni pamoja
na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na wengine wastaafu.
“Hatuna uhakika na viongozi wengine kutoka nje ya nchi maana mwaliko umetoka
kwa muda mfupi, lakini mabalozi waliopo nchini wote tumewaalika na makundi
mengine yote kama wakulima, wasanii, wavuvi, wafugaji na kila anayeguswa na
Katiba mwakilishi wake lazima atakuwapo,” alisema Dk Nchimbi.
Kuhusu orodha kamili ya waalikwa
alisema: “Kesho (leo) naweza kuwa na majibu mazuri kwa kila kitu maana
tunashirikiana na vyombo vingine katika kazi hii, kwa hiyo nitawaambia kwani
vikao bado vinaendelea.”
Awali, Naibu Katibu wa lililokuwa
Bunge la Katiba, Dk Thomas Kashililah alisema maandalizi ya sherehe hiyo
yamefanyika chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
EmoticonEmoticon