NA NASRA ABDALLAH, Dar Es Salaam
VIJANA nchini wametakiwa kujitokeza kuwania
nafasi za uongozi ikiwamo nafasi za juu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar
es Salaam na Katibu wa Chama cha Walimu wa somo la Uraia (CETA), Safari Minja,
katika warsha ya siku moja ya kuwajengea uwezo vijana kuhusu haki na wajibu wao
katika uchaguzi.
Minja, alisema vijana wengi wamekuwa wakiwaachia
watu wazima kugombea nafasi ya Uenyekiti na wao kubaki mashabiki, jambo ambalo
alidai wanapaswa kubadili tabia hiyo.
Pia, alionya kuhusu suala zima la upigaji kura,
kwani vijana wamekuwa wakishiriki katika kampeni kwa wingi lakini inapokuja
hatua ya kupiga kura wanaingia mitini na hivyo kujikuta wakijinyima haki yao ya
kuchagua au kuchaguliwa viongozi ambao sio hitaji lao.
Kuhusu umri wa vijana chini ya miaka 40, alisema
hata yeye haungi mkono na kufurahishwa kuondolewa kipengele hicho.
Mojawapo ya sababu alizozitaja, kuwa ni hatari
endapo sheria hiyo ingepitishwa, kwani kijana chini ya umri huo anakuwa bado
hajakomaa kimaono, kiakilii, kijamii na kifamilia.
Kwa upande wake, mmoja wa kijana aliyehudhuria
warsha hiyo, Nelson Kasena, alisema wameweza kupata uelewa wa mambo mbalimbali
ambayo walikuwa hawayajui kuhusu taratibu za uchaguzi.
Kasena, alisema kati ya jambo lililomvutia ni
uandikishaji kwa njia ya kielektroniki na kuongeza kuwa, bado elimu zaidi
inatakiwa kuhusu mfumo huo ambao bado ni mgeni hapa nchini.
Naye Mwakilishi kutoka shirika la Kijerumani la
Konrad Adenauer Stiftung, ambao ndio waliwezesha kufanyika kwa wa warsha hiyo,
Sefan Reith, alisema vijana hawana budi kupewa elimu ya uraia mara kwa mara,
kwa kuwa ndio viongozi wajao wa taifa hili.
EmoticonEmoticon