Dodoma.TANZANIA
Kauli ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,
Samuel Sitta kwamba fedha ambazo
zitakuwa zimeokolewa katika siku 60 za uendeshaji wa Bunge hilo hazitarejeshwa
serikalini, bali zitatafutiwa utaratibu wa namna ya kuzitumia, imemgonganisha
na katibu wake, Yahya Khamis Hamad ambaye amesema “hilo ni jambo la ajabu”.
Sitta alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati
akiahirisha Bunge hilo lenye wajumbe 500 baada ya wajumbe 130 wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kulisusia tangu Aprili 16, mwaka huu.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh300,000
kwa siku sawa na Sh150 milioni kwa siku kwa wajumbe wote, huku Serikali ikiwa
imetenga Sh20 bilioni kwa ajili ya siku 60 za uendeshaji wa Bunge hilo.
Kauli hiyo ya Sitta kuwa fedha zitakazookolewa
zitatafutiwa utaratibu badala ya kurudishwa zilikotoka, iliwafanya wajumbe wa
Bunge hilo kulipuka kwa furaha na kugonga meza.
Hata hivyo, katibu wa Bunge, Yahya Khamis Hamad
alishangazwa na kauli hiyo ya Sitta akisema: “Mimi hayo niliyasikia lakini
kwangu pia ni ya ajabu kwa sababu fedha tulizonazo hazitoshi, sasa hizo za
kubaki mimi sijui.”
Katibu huyo alisema kwa sasa, Wizara ya Fedha
inawapa kiasi cha fedha kwa kile tu ambacho kinahitajika na yeye anatoa taarifa
serikalini kwa kiasi kilichotumika. “Mimi sijui labda yeye anajua sitaki
kumsemea,” alisema.
Sitta pia aliwaeleza wajumbe hao kuwa baada ya
kukabidhi Katiba inayopendekezwa, wote watakabidhiwa cheti na Rais Jakaya
Kikwete.
“Cheti hicho kitakuwa na sahihi ya Rais mwenyewe
kwa hiyo tutakaa kidogo kusubirisubiri Katiba iliyokamilika, haiwezi kuwa ya ovyo
ovyo tu lazima iwe na viwango vizuri,” alisema Sitta na kuongeza:
“Tutachapisha nakala nyingi kila mmoja aende na
waraka huo wa kihistoria nyumbani na itakuwa ni Katiba bora sana hapa Afrika na
Kusini mwa Sahara.”
Mwenyekiti huyo aliwapiga vijembe viongozi wa
Ukawa na makundi mengine yanayopaza sauti kutaka Bunge hilo lisitishwe ili
kuokoa pesa
“Tutamaliza zoezi hilo Oktoba 3, mwaka huu ili
tutoke na Katiba inayopendekezwa kinyume na wale wanaopiga kelele ovyo bila
kuwa na sayansi kichwani eti unaokoa gharama kwa kusitisha mchakato.
“Mchakato huu ungesitishwa ina maana utawala
ujao, rais ajaye ingembidi kuanza upya na Tume na aingie tena kwenye Bunge
Maalumu la Katiba,” alisema Sitta.
EmoticonEmoticon