LICHA
ya kuwa na Madaktari bingwa wa upasuaji wa kichwa wasiozidi watano tu nchini,
wodi za kitengo cha upasuaji wa kichwa na mifupa cha Hospitali ya Rufaa ya
Taifa Mhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam, zimefurika wagonjwa.
Mratibu wa jopo la madakatari bingwa saba wa MOI
walioweka kambi maalum ya matibabu ya mgongo na upasuaji kichwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) jijini Mwanza, Dkt Othman Kiloloma, amesema
hali hiyo ni moja ya changamoto kubwa inayokikabili kitengo hicho.
Amedai, kutokana na kusubiri matibabu hayo kwa
muda mrefu, baadhi ya wagonjwa wa nje ya Dar es salaam huishiwa fedha za
kujikimu na hata nauli, hivyo Madkatari hao kulazimika kuwasaidiwa nauli za
kuwarudisha makwao.
Dkt Kiloloma alisema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya uzinduzi wa Matibabu ya
mgongo na upasuaji kichwa unaofanywa na wataalam hao hapa, kwa kushirikiana na
madakatari bingwa wa BMC.
Matibabu hayo yanayotolewa bure kwa ufadhili wa
kampuni ya African Barrick Gold katika hospitali ya Bugando, yalianza juzi
(Machi 24) na yataendelea hadi Machi 28 mwaka huu ambapo wagonjwa zaidi 33
wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa vichwa na kutibiwa migongo.
“Wodi
zetu zimejaa wagonjwa wetu wanasubiri kwa muda mrefu, ukituletea mgonjwa
atalala wapi wakati wamejaa hadi kwenye makorido lakini hatuwezi kuwafukuza.”
Alieleza Dkt Kiloloma wakati akionyesha picha za wagonjwa waliolazwa MOI,
walivyofurika.
Alisema kupeleka wagonjwa wa aina hiyo Dar ni
gharama kubwa hivyo ndiyo maana jopo hilo kwa ufadhili wa kampuni hiyo ya
uchimbaji madini nchini, limeweka kambi Bugando ili kuwasaidia wagonjwa waliopo
kanda ya ziwa ambao ingebidi wapelekwe Mhimbili au nje ya nchi kwa matibabu
hayo.
“Kati
ya Madaktari saba tuliotoka MOI kuja Mwanza kuungana na wenetu wa Bugando
kusaidia wangonjwa wa Kanda hii ya ziwa, mabingwa wa upasuaji wa kichwa tupo
watatu. Tanzania nzima ina mabingwa wa Upasuaji kichwa wasiozidi watano, hivyo
wawili ndio wamebaki Dar.” Alieleza bingwa huyo na kudai
upungufu wa wataalamu hao ni changamoto kubwa inayolikabili taifa.
Alieleza kwamba kukamilika kwa jengo la ghorofa
nane linalojengwa MOI kutasaidia kuondoa mlundikano wa wagonjwa ambao sasa
wanakosa pa kulala licha ya wengine kuwa nje ya wodi wakisubiri matibabu.
“Tunapasua
wagonjwa 600 kwa mwezi lakini kutokana na kusubiri matibabu kwa muda mrefu
kidogo, baadhi au wauguzi wao huishiwa fedha za kujikimu na kulazimika
kuwasaidia nauli ya kurudi kwao, wengine (akina mama) hukuta waume zao walisha
oa wanawake wengine.” Alidai.
CREDIT: G-SENGO