REPIN ROCK CITY

REPIN ROCK CITY

TUMA TRACK YAKO

TAARIFA: ABSALOM KIBANDA AMEATHIRIKA SANA....

4:17:00 AM

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Halima Mlacha na Lucy Lyatuu



BAADA ya uchunguzi wa awali wa madaktari katika Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam kubaini kwamba Mhariri Mtendaji wa New Habari Corporation, Absalom Kibanda mbali na kujeruhiwa kichwani, kung’olewa meno, kucha na kukatwa kidole, zimebainika athari nyingine kwake.

Uchunguzi uliofanywa jana na madaktari wa Hospitali ya Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini alikolazwa, umeonesha kuwa mbali na hayo, fizi kati ya pua na kinywa imekatika kutokana na nguvu na nyenzo walizotumia watesaji wake kumng’oa meno na kumsababishia maumivu makali.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena akikariri taarifa za Johannesburg, ilisema Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa TEF, meno yake sita yamelegea.

Ilisema tangu awasili jana Milpark, amekuwa akiendelea na matibabu kwa maana ya kufanyiwa vipimo vikiwamo vya CT Scan na X Ray hasa kichwani na sehemu nyingine za mwili ambazo zilipata majeraha.

“Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, jopo la madaktari wenye ujuzi wa aina tofauti, walikuwa wakitarajiwa kukutana ili kusoma taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo, ili kutafsiri maana ya matokeo hayo, kisha kutoa mwelekeo wa nini kinafuata au aina ya tiba anayopaswa kupata,” ilisema taarifa.

Jana uongozi wa Jukwaa la Habari za Kiuchunguzi la Afrika Kusini ulimtembelea Kibanda hospitalini Milpark na kueleza masikitiko yake kuhusu yaliyomkuta.

Waliahidi kushirikiana na taasisi za kihabari za Tanzania, kuchunguza tukio hilo kwa lengo la kupata majawabu ya nini kilichojiri na sababu za unyama huo.

Akizungumza na gazeti hili jana mchana, mke wa Kibanda, Angela Semaya alisema kwa mujibu wa muuguzi anayemshughulikia mumewe, walikuwa wakimsubiri daktari na wataalamu wengine ili kusoma vipimo kujua kiwango cha athari.

Alisema baada ya kusoma vipimo na kujua alivyoathirika ataanza matibabu ya jumla. Semaya alisema kwa sasa mumewe anaendelea vizuri kwani ana kumbukumbu zote, lakini mara nyingine analalamika maumivu sehemu alizojeruhiwa.

Kituo chalaani Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimesema kimepokea kwa mshituko na mshangao taarifa za kuvamiwa na kushambuliwa kwa Kibanda na kulaani wahusika na tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kituo hicho, James Mbatia, aliliita tukio hilo kuwa ni ovu na la kiharamia lisilopaswa kuvumiliwa.

“Kikao chetu cha TCD kinatoa pole nyingi kwa ndugu wa Kibanda na kumwombea heri aweze kupona haraka ili aendelee na majukumu yake. Lakini pia tunalaani kwa nguvu zote tukio hili,” alisema Mbatia.

Alisema kituo hicho kinavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo kwa haraka ili wahusika wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.

“Lakini tunasisitiza kuwa Serikali iwe makini zaidi kukomesha matukio ya namna hii ambayo yameanza kukithiri nchini, kwani yanajenga wasiwasi, chuki, uhasama na hasira miongoni mwa raia wa Tanzania na kuhatarisha usalama wa amani ya nchi yetu,” alisema.

Warioba azungumzia Naye Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba alisema ni tukio linaloleta wasiwasi katika jamii na kutaka wananchi kushirikiana na Polisi katika kuyatokomeza.

Alisema tukio hilo linaonesha kuwa si la kijambazi ni kisasi cha kukomoana na ambayo yanaweza kuleta hatari kubwa katika jamii. “Tukio hili si la ujambazi ni la kulipiza kisasi cha kukomoana … yanatakiwa kudhibitiwa, kwani tofauti na hivyo yatakuwa hatari sana katika jamii,” alisema Warioba.

Kibanda alivamiwa saa sita usiku wa kuamkia juzi, nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake wakati akirejea nyumbani akitoka kazini na alitobolewa jicho, kung’olewa meno, kukatwa kidole cha mkono, kupigwa mapanga mguuni, kupigwa na nondo kichwani na mikononi ambapo wavamizi hawakuchukua chochote.

Kabla ya kusafirishwa nchini Afrika Kusini alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »

MNADA BANNER