Kamanda wa Polisi wa Mkoa Maalum wa Tarime Rorya, JUSTUS KAMUGISHA
Na Samson Chacha, Tarime
MKAZI wa Kijiji cha Genkuru, Marwa George (38), anadaiwa
kuuawa kwa kuchomwa mkuki kwenye paja la kushoto na baba mkwe, John Mhabe (67).
Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika Kijiji cha
Kitawasi, anakoishi baba mkwe huyo, baada ya George kwenda kudai mahari
aliyotoa ili kuoa kwenye nyumba hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Maalumu wa Tarime Rorya, Justus
Kamugisha, alisema jana kuwa George alipooa, alitoa mahari ya ng’ombe 10.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, miaka mitatu
iliyopita, George alikimbiwa na mkewe huyo ambaye jina lake halijapatikana,
kutokana na migogoro ya ndani, ambayo haikufafanuliwa na inasemekana, alikwenda
Geita na kujiunga na wachimbaji wadogo wa dhahabu.
Alisema baada ya kukimbiwa na mkewe, George alikwenda kudai
ng’ombe aliotoa kama mahari na alipofika nyumbani kwa baba mkwe, moja kwa moja
aliingia zizini na kuchagua ng’ombe.
Inadaiwa alichagua mafahari watano na kuwatoa zizini ingawa
baadhi ya mashuhuda wakati akiwatoa mafahari hao walimsihi kuacha kitendo
hicho, lakini alikaidi na kuwaswaga kuelekea kwake.
Wakati akiondoka nao, inadaiwa baba mkwe alikasirika na
kuchukua mkuki na kumchoma kwenye paja la kushoto na kumsababishia kuvuja damu
nyingi na kufariki dunia.
Kamanda Kamugisha alisema Polisi inamshikilia mtuhumiwa huyo
na baada ya mahojiano, anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya
mauaji.
Tayari mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi na
kuchukuliwa na ndugu zake kwa mazishi kijijini kwake Genkuru.
Kamanda Kamugisha alitaka wananchi kutojichukulia sheria
mkononi, badala yake wafuate sheria na kupunguza hasira wakati wakitaka
kuchukua uamuzi.
Aliwataka kama watashindwa kudhibiti hasira, washirikishe
wana ndugu badala ya kujiamulia, ili kuepuka maafa kama hayo.
EmoticonEmoticon