Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, limesema liko mbioni
kupata ‘mwarobaini’ kwa wananchi wanaotoa taarifa za udanganyifu na lugha za
matusi kwa kupiga simu za uongo kwa jeshi hilo .
Jeshi hilo
limesema katika kukabiliana na hali hiyo, litafunga mtambo wa kuwabaini
wahusika hao.
Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini,
Jenerali Saimon Mgomba, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar
es Salaam wakati akiwatunuku vyeo maofisa tisa wa jeshi hilo .
Alisema changamoto kubwa inayolikabili Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji nchini ni kupokea taarifa za uongo kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa
kuna tukio la moto.
Mgomba alisema jeshi hilo
hupokea wastani wa taarifa za simu za uongo 20 kwa siku kwamba kuna matukio ya
moto yametokea katika maeneo fulani.
Aliongeza kuwa mbali na kuwapo kwa miito ya uongo, pia
hupokea lugha za matusi kutoka kwa baadhi ya wananchi. “Haya ni mateso makubwa
tunayoyapata, nasema siku zao zinahesabika ndani ya wiki mbili hadi tatu
tutafunga mtambo wa kuzijua namba hizo pamoja na majina yao ,” alisema Mgomba.
Alisema zoezi hilo litaanzia Dar es Salaam na litakuwa
endelevu katika mikoa mingine muda mfupi ujao.
Aidha, alisema malengo ya Jeshi la Zimamoto kwa sasa ni
kufika katika eneo la tukio ndani ya dakika 15 lakini wanakwamishwa na tatizo
la miundombinu ya Jiji la Dar es
Salaam kutokana na foleni.
Pia alisema tatizo la visima vya kuchotea maji bado ni
changamoto na kueleza kuwa hadi sasa wana visima vitano vinavyofanya kazi na
zaidi ya 1,000 vibovu.
EmoticonEmoticon