Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), wiki hii kinatarajia kumburuza mahakamani, Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, kumtaka afute kauli yake aliyoitoa bungeni mwezi uliopita
kwamba Polisi wawapige raia wanaoleta uchokozi na kuashiria uvunjifu wa amani
hapa nchini.
Mwezi uliopita Pinda katika mkutano wa Bunge la bajeti mjini
Dodoma alitoa kauli ya kulitaka jeshi la Polisi
nchini kuwapiga raia wanaokaidi amri halali ya jeshi hilo wakati aikijibu maswali ya Papo kwa papo
kwa Waziri Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana jijini
Dar es Salaam ,
Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia, alisema taratibu
zote za kisheria za kumfikisha Pinda mahakamani zimekamilika na siku yoyote
wiki hii watafungua kesi.
Sungusia alisema kauli ya Pinda, imevunja katiba ibara ya 13
na kwamba lazima sheria ichukue mkondo wake kwa mkumfikisha mbele ya mahakama.
Alifafanua kuwa ibara ya 100 inayompa kinga mbunge anapotoa
jambo lolote bungeni inamweka kando Pinda, kwa kuwa yeye hakuzungumza bungeni kama mbunge bali alikuwa anatoa msimamo wa serikali yake.
Alisema kauli ya
Pinda ilikuwa kali na mbaya na kwamba, walimtaka Pinda aifute siku chache baada
ya kuitoa, lakini mpaka sasa amekaidi na hivyo wameamua kuchukua hatua ya
kumfikisha mahakamani ili haki iweze kutendeka.
Pinda alitoa kauli hiyo nzito alipokuwa akijibu swali la
mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyetaka kujua kauli ya
serikali juu ya vyombo vya dola kudaiwa kuwapiga raia hususani katika mikoa ya
Mtwara na Arusha.
Akijibu swali hilo
Pinda alisema “Mheshimiwa Mangungu hapa ameanza vizuri, lakini mwisho hapa
naona anasema vyombo vya dola vinapiga watu, ukifanya fujo au umeambiwa
usifanye hiki ukaamua kukaidi utapigwa tu.”
Akaendelea kusema
kuwa, “Lazima wote tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya sheria
na kama wewe umekaidi, unaona kwamba ni imara
zaidi, wewe ndio jeuri zaidi, watakupiga tu,"
“Na mimi nasema wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi
muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine ya kupambana na wakaidi zaidi ya
kuwapiga,” alisema Pinda.
T.A.T NIPASHE
EmoticonEmoticon