MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA) imekamata magari 70 ya abiria kutokana na kufanya makosa mbalimbali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana
kuhusu kero mbalimbali zinazowakabili wananchi, Ofisa Mfawidhi Kanda ya
Mashariki wa SUMATRA , Conrad Shiyo, alisema
magari hayo yamekamatwa kuanzia juzi na miongoni mwa makosa yaliyosababisha
yakamatwe ni kutumia tiketi za bei ya zamani huku wakiwatoza abiria bei mpya,
kitendo ambacho ni sawa na kuwaibia.
“Tumegawa chati za bei kuanzia Jumatatu kwa kila gari, zenye
utambuzi wa bei ya nauli za zamani na mpya hivyo kila mwananchi anayo haki ya
kuoneshwa chati hiyo pindi anapotaka na akinyimwa kuiona hilo ni kosa na mhusika atachukuliwa hatua,”
alisema Shio.
Alisema mamlaka hiyo pia itakamata madereva ambao
wataendesha magari ambayo hayajafuta bei ya zamani ubavuni mwa magari yao na magari yote yatakayokamatwa kwa makosa mbalimbali
yatawekwa katika yadi ya mamlaka hiyo na kusubiri uamuzi wa mkurugenzi kama atayafuta kabisa au la.
Alisema nia ya mamlaka hiyo ni kuboresha hali ya usafiri
katika kila pembe ya jiji ili kila abiria aweze kusafiri na kufika anakokusudia
bila ya vikwazo vinavyotokana na tamaa za watu wasiotosheka na wanachokipata
kihalali.
Pamoja na mambo mengine alisema hivi karibuni alikutana na
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani katika kupanga mikakati
ya kuyakamata magari yote yaliyosajiliwa kwa ajili ya kutoa huduma kati ya
mikoa hiyo na kunyang’anywa leseni.
EmoticonEmoticon