Na Vicky Ntetema
HALI ya wasiwasi imetanda miongoni mwa watu wenye ulemavu wa
ngozi (albino) nchini, baada ya watu watatu kukatwa viungo na mmoja wao kuuawa
mwezi huu.
Katika miaka ya hivi karibuni, jumla ya albino 72 wameuawa,
34 wamenusurika, wengi wao kwa kukatwa viungo au kuumizwa. Makaburi 15
yamefukuliwa na viungo kuchukuliwa na kumekuwa na majaribio manne ya kufukua
makaburi.
Katika matukio ya hivi karibuni, walemavu hao wakazi wa
Tabora na Sumbawanga wamekatwa mikono ya kushoto. Ukatili huo safari hii
umekwenda kinyume na ilivyokuwa mwaka 2010-2011 wakati mikono ya kuume ndiyo
iliyokuwa inakisiwa.
Aliyeuawa ni
Lugolola Bunzari (7) na waliojeruhiwa ni Mwigulu Matonange
(10) na Maria Chambanenge (39).
Katika matukio hayo, mtoto mwenye umri wa miezi saba
alinusurika kuuawa baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba ya mama yake
usiku katika eneo la Lamadi, Wilaya ya Busega, Mwanza siku moja baada ya
kupokea ujumbe mfupi wa simu kwamba mtoto wake anawindwa.
Marehemu Lugolola
Kijiji cha Kanoge kina umbali wa takriban kilomita 75 kutoka
Tabora Mjini, barabara iendayo Ulyankulu kwenye machimbo ya dhahabu.
Imenichukua saa mbili na nusu kufika huko. Saa moja na nusu
kati ya hizo, nilizitumia katika safari ya kilomita 15 tu kutoka Kanoge makao
makuu ya kijiji hadi Kitongoji cha Kinondoni alikouawa mtoto Lugolola.
Nyumbani kwa Bunzari niliwakuta ndugu na jamaa kutoka vijiji
vya jirani vya Wilaya hiyo ya Kaliua, Tabora. Bibi mzaa baba wa Lugolola, Gama
Zengabuyanda (60), ndiyo kwanza alikuwa amerejea kutoka Hospitali ya Mkoa ya
Kitete alikokuwa akitibiwa baada ya kushambuliwa na majambazi alipotaka
kumwokoa mjukuu wake.
Huku akilia kwa huzuni, Zengabuyanda alinisimulia jinsi
mjukuu wake na baba yake mzazi, Zengabuyanda Meli (95) walivyouawa kikatili.
Katika muda wa kati ya saa 10 na 11 alfajiri ya kuamkia
Februari Mosi mwaka huu, Lugolola aliuawa kikatili baada ya kukatwa mkono kwa
panga, kukwanguliwa nywele, kujeruhiwa mkono wa kulia na sikioni na kuondolewa
ngozi kwenye sehemu ya paji la uso.
Katika mashambulizi hayo, babu yake Meli pia aliuawa
alipojaribu kumwokoa mjukuu wake. Vilevile baba yake mzazi, Bunzari Shinga
alijeruhiwa wakati alipojaribu kumlinda mwanaye.
Nilimkuta mama mzazi wa Lugolola aitwaye Kulwa akisaidiana
na ndugu zake kumenya maharage mabichi waliyoyatoa shambani mwao muda mfupi tu
uliopita.
Yeye ni mke mkubwa wa Bunzari Shinga (35). Walibahatika
kupata watoto sita, wawili kati yao
ni albino. Lugolola na marehemu mdogo wake aitwaye Maganga aliyefariki kwa
malaria mwaka 2011.
Usiku wa mashambulizi hayo, Kulwa anasema alikuwa amelala na
watoto wake wadogo wa kike (mmoja, Shija mkubwa) na Lugolola kwenye nyumba yake
inayotazamana na ile ya mke mwenzake Pili, umbali wa takriban mita 20. Bunzari
alikuwa amelala kwa mke huyo mdogo na binti yao mwenye umri wa mwaka mmoja hivi.
Mzee Meli alikuwa amelala na watoto wa kiume upande wa kulia
wa nyumba ya Kulwa.
“Aliamshwa usingizini na kelele za watoto waliokuwa
wakilalamika kwamba wanapigwa na fimbo. Alipotaka kwenda chumbani kwa watoto
alishambuliwa kwa mapanga kichwani, usoni, mgongoni, mikononi na miguuni,” Gama
anaelezea huku akilia.
EmoticonEmoticon