NEW YORK, MAREKANI
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya
kibinaadamu amezitaka nchi za Kiafrika kuongeza juhudi za kupambana na tatizo
la chakula na vile vile kusimama imara katika kukabiliana na majanga ya
kimaumbile.
Catherine Bragg amesema hayo mwishoni mwa safari yake katika eneo
la kusini mwa Afrika na kuonya kuwa, eneo la kusini mwa Afrika linakabiliwa na
tatizo sugu la chakula na kwamba, uzalishaji chakula katika eneo hilo
umedhoofika kutokana na majanga mtawalia ya kimaumbile.
Amesema, theluthi moja
ya wananchi wa Lesotho hawana uwezo wa kukidhi mahitaji yao ya chakula.
Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinaadamu amebainisha
kwamba, nchini Zimbabwe raia milioni moja na laki sita wanakabiliwa na hatari
ya tatizo la chakula na kwamba, familia nyingi zimekuwa zikiuza mifugo yao ili
ziweze kukidhi mahitaji yao ya chakula.
Ofisi ya Uratibu wa masuala ya
Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa taarifa inayobainisha kwamba, suala la
tatizo la chakula lingali tatizo kubwa katika eneo la kusini mwa Afrika hususan
katika nchi za Lesotho, Malawi, Swaziland na Zimbabwe.
EmoticonEmoticon