SONGEA, Tanzania
Idadi ya watu waliolazwa hospitalini kwa kunywa
togwa inayosadikiwa kuwa na sumu katika Kijiji cha Litapwasi, Kata ya Mpitimbi
mkoani Ruvuma imeongezeka kutoka 270 hadi 340.
Tukio hilo lilitokea Jumapili baada ya watu
kushiriki sherehe ya Kipaimara ambako walikula, kunywa pombe na togwa na
baadaye wale waliokunywa togwa walianza kuumwa matumbo, kuhara na kutapika.
Hadi jana, watu 102 walikuwa bado wamelazwa
katika Zahanati ya Lyangweni, Hospitali ya St. Joseph Peramiho na Hospitali ya
Mkoa wa Ruvuma.
Tayari watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa
upelelezi kuhusiana na tukio hilo, akiwamo Baba Mzazi wa mtoto Dickson
aliyepata kipaimara, Enes Nungu (47).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo
Mskhiela aliwataja watu wengine wanaoshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi
Songea kwa mahojiano kuwa ni Benedict Nungu (76), Esebius Komba (36), Sadiki
Masodi (65) na John Kaulangudidi. Mtu anayedaiwa kukabidhiwa ufunguo chumba cha
vinywaji kabla ya kugawiwa kwa wananchi, Ridhiwani Shawa haijulikani alipo.
Mabaki ya chakula, togwa na pombe ya kienyeji
vilichukuliwa juzi na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Kamanda Mskhiela alitoa wito kwa wananchi
wanaoandaa sherehe kuhakikisha wanafanya hivyo katika mazingira mazuri na yenye
usalama ili kuepuka athari kama hizo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Peramiho, Dk Vanace
Mushi alisema hadi jana, watu waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo
walikuwa 34 na hakukuwa na mgonjwa aliyeruhusiwa kurudi nyumbani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa
Ruvuma, Majuto Mlawa alisema wagonjwa tisa wa rufaa walipokewa na kupatiwa
matibabu huku hali zao zikiwa mbaya.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,
Said Mwambungu alisema: "Jambo hili limenisikitisha sana, nimeumizwa sana
nawapa pole wote waliopatwa na tatizo hilo naamini Mwenyezi Mungu atawasaidia
na watapona na kurejea katika hali zao za kawaida."
Hata hivyo, Mwambungu alisema hiyo ni ajali kama
nyingine, hivyo anaviachia vyombo vya usalama na wataalamu wa afya kupata
ukweli. Pia aliwataka wananchi kuwa makini pindi wanapoandaa vyakula na pombe
za kienyeji katika sherehe mbalimbali.
Chanzo:Mwananchi
EmoticonEmoticon