KUTOKA Arusha, TANZANIA
Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa mashahidi wanaotarajiwa
kuitwa na walalamikaji katika shauri dhidi ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda
linaloendelea katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).
Wakili Jimmy Obeid anayewawakilisha walalamikaji katika shauri
namba 9/2013, jana aliieleza Mahakama kuwa miongoni mwa mashahidi watakaoitwa
kujenga kesi hiyo ni pamoja na Rais Kikwete.
Shauri hilo lilifungulliwa na Watanzania watatu, Ally Hatib
Msangi, David Makatha na John Bwenda wakidai kitendo cha Kenya, Uganda na
Rwanda kufanya vikao bila kuzishirikisha Tanzania na Burundi ni ukiukwaji wa
mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
Miongoni mwa vifungu vya mkataba wa EAC vinavyodaiwa kukiukwa ni
namba 3(3) (c) kinachotaka ushiriki sahihi kuimarisha ushirikiano ndani ya
ukanda wa Afrika Mashariki na Kifungu cha 6 (a) (b) (d) na (f) kinachozitaka
nchi wanachama kuzingatia misingi ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Katika ushahidi wake, Rais Kikwete ataombwa kuthibitisha hotuba
yake kwa Taifa aliyoitoa bungeni Novemba 7, mwaka jana ambayo ilielezea jinsi
Tanzania na Burundi zilivyotengwa na baadhi ya nchi wanachama wa EAC.
“Kutokana na uzito na majukumu ya Rais Kikwete tunayepanga
kumwita kama mmoja wa mashahidi wetu, naiomba Mahakama muda wa mwezi mmoja
kuwasilisha orodha ya mashahidi na hati za viapo,” alisema Obeid. Jopo la
majaji watano wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Jean-Bosco Butasi, Naibu Jaji
Kiongozi, Isaac Lenaola na wengine Faustin Ntezilyayo, Monica Mugenyi na Fakhi
Jundu walikubali ombi hilo na kupanga Oktoba 24, mwaka huu wadai kuwasilisha
hati ya kiapo na orodha ya mashahidi.
Wadaiwa katika shauri hilo ni Katibu Mkuu wa EAC,
anayewakilishwa na wakili Dk Antony Kafumbe wakati mdaiwa wa pili ni
Mwanasheria Mkuu wa Kenya anayewakilishwa na mawakili wawili, Muthoni Kimani na
Peter Ngumi, mdaiwa wa tatu ni Mwanasheria Mkuu wa Uganda anayewakilishwa na
mawakili watatu, Elisha Bafirawala, Richard Adrole na Maureen Ijang’ na mdaiwa
wa nne ni Mwanasheria Mkuu wa Rwanda anayewakilishwa na wakili Malaala Aimable.
Wadaiwa hao watawasilisha majibu kabla ya Novemba 7 mwaka huu na
kutoa maelezo ya ziada Novemba 14 mwaka huu kabla ya Mahakama kupanga siku ya
shauri hilo kusikilizwa na pande zote zitapewa wito maalumu.
Septemba 2, mwaka huu, wadai waliondoa mahakamani ombi la zuio
la muda dhidi ya vikao vya muungano wa wenye nia (coalition of the willing),
baada ya Tanzania na Burundi kuanza kushirikishwa kwenye vikao viwili
vilivyofanyika Februari 24 na Mei 2, mwaka huu.
EmoticonEmoticon