Sakata la kutupwa kwa viungo vya
binadamu bila kufuata utaratibu jana liligeuka sinema wakati maofisa wanne wa
Chuo Kikuu cha Tiba na Teknolojia (IMTU), walipofikishwa mahakamani Dar es
Salaam.
Maofisa
hao ambao ni maprofesa na wahadhiri wa chuo hicho walifikishwa katika Mahakama
ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kushindwa
kufukia viroba 83 vya miili ya binadamu.
Baada ya
mashtaka hayo kusomwa na taratibu za dhamana kukamilika huku mmoja wao
akishindwa kutimiza masharti, watuhumiwa hao walirejeshwa kizimbani na kufutiwa
mashtaka hayo kwa amri ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) aliyewasilisha hati ya
kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo.
Hata
hivyo, furaha waliyoipata washtakiwa hao, Venkat Subbaiah (57), Appm Shankar
Rao (64), Prabhakar Rai (69) na Dinesh Kumar (27) ilikuwa ya muda tu,
kwani polisi waliokuwapo mahakamani hapo waliwakamata tena na kuondoka nao.
Hati ya
mashtaka
Akiwasomea
mashtaka, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Polisi, Magoma Mtani alidai kuwa
washtakiwa hao Julai 2014 katika eneo la Mpigi Majohe, walishindwa kufukia
viroba 83 vya miili ya binadamu waliyoitumia kufundishia wanafunzi wa udaktari
kinyume na Kifungu cha 128 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka
2002.
Alidai
kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kuandaa hati ya ofisa mchunguzi wa
vifo vyenye mashtaka (coroner).
Baada ya
kusomewa mashtaka hayo watuhumiwa wote waliyakana na upande wa mashtaka ulidai
kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu
Mwandamizi wa mahakama hiyo, Kwey Rusemwa alitoa masharti ya dhamana akiwataka
kila mmoja wao kuwa na wadhamini wawili ambao ni raia wa Tanzania na wanaofanya
kazi kwenye taasisi zinazotambulika kisheria.
Washtakiwa
watatu walikamilisha masharti hayo lakini mmoja alishindwa kutokana na kuwa na
mdhamini ambaye si raia wa Tanzania.
Mashtaka
yafutwa
Wakati
washtakiwa hao wakikamilisha taratibu za dhamana wakiwa ndani ya mahakama hiyo,
Wakili wa Serikali, Salum Ahmed aliingia na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo
chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) kwa kuwa
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.
EmoticonEmoticon