Wabunge wanne wa Chadema, Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu
Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti
Maalumu) wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mkusanyiko usio halali kwenye
Uwanja wa Soweto jana.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema
jana kwamba pamoja na wabunge hao pia wamewakamata watu wapatao 60 kutokana na
vurugu zilizozuka jana baada ya Polisi kuwatawanya kwenye uwanja huo waliokuwa
wamekusanyika kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na
Amir Ally waliofariki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea kwenye uwanja huohuo,
Jumamosi iliyopita.
Mbali ya viongozi hao, alisema wanawasaka Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
“Tunawasaka wabunge ili tuwajumuishe na watu hawa kwa kosa
la kuhusika na mkusanyiko usiokuwa halali. Hadi sasa tumefanikiwa kulinasa gari
la Mbowe,” alisema Chagonja.
Pia kamatakamata hiyo imemkumba Mpigapicha wa Kituo cha
Televisheni cha Channel Ten, Ashraf Bakari. Polisi walilazimika kutumia nguvu
kuwatawanya waombolezaji hao.
Awali, Kamishna Chagonja alisema jana asubuhi kuwa
wamelazimika kuzuia viwanja hivyo kutumika baada ya wamiliki wake, AICC kuzuia
shughuli za Chadema kwenye eneo lao na kwamba upelelezi bado unaendelea katika
viwanja hivyo.
Kamishna Chagonja aliwaonyesha waandishi wa habari barua
aliyosema imeandikwa na uongozi wa AICC kuzua Chadema kuendelea kuutumia Uwanja
wa Soweto.
Mabomu yarindima
Dalili za kuzuka kwa vurugu zilianza kuonekana asubuhi baada
ya polisi kuzingira uwanja huo na kuzuia watu waliokuwa wameanza kufurika
katika eneo hilo kuanzia saa moja kuingia kwa ajili ya maombolezo.
Wakati Polisi wakiwa uwanjani, wananchi walijaa nje ya
uwanja na kuonekana kama wamewazingira.
Viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe waliwasili uwanja
hapo yapata saa nane mchana na kukuta zuio hilo na kuanza kuzungumza na
wananchi ingawa FFU walikuwa wakiwataka watu kutawanyika. Mabomu yalianza
kurindima wakati Arfi aliposimama na kuwahimiza wananchi kuelekea Hospitali ya
Mount Meru kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu.
“Tuna muda mfupi sana wa kuzungumza hapa, tunaomba wote
tuelekee Hospitali ya Mount Meru kuaga miili ya marehemu kwa sababu uwanja huu
umezuiwa na polisi,” alisema Arfi kabla ya kukatishwa na milipuko ya mabomu.
Awali, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema alitoa
msimamo wa chama hicho kuwa Mwenyekiti wao, Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wa
tukio la bomu wala kujisalimisha polisi kwa sababu hawana imani na jeshi hilo.
“Namtaka Chagonja atangulie mahakamani, tutakutana hukohuko.
Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wala kujisalimisha polisi... ” alisema Lissu
na kuongeza:
“Kisheria haiwezekani polisi ambao ndiyo watuhumiwa ndiyo
wadai kukabidhiwa ushahidi ili wauharibu.”
Mapema Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kutoa
ushahidi wa polisi kuhusika na tukio la kurusha bomu kwenye mkutano wa Chadema
la sivyo polisi watatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo.
Hekaheka
Baada ya polisi kuanza kutupa mabomu saa 8.45 mchana,
wabunge, viongozi waandamizi wa Chadema na watu waliokuwa wamekusanyika
walilazimika kutimua mbio.
Watu walioshuhudia tukio lile wanasema viongozi hao akiwamo
Mbowe na mwenzake Lissu walikimbilia kwenye magari yao. Lema alilazimika
kukimbilia kwa wachoma nyama ya nguruwe, (kitimoto) kwenye maeneo ya Kaloleni.
Kabla ya polisi kurusha bomu mahali alipokuwapo Lema, mbunge
huyo alisikika akisema:
“Jaribuni kuvumilia, tunajaribu kuwasiliana Serikali ya
Mkoa, ili watupe kibali cha kuleta miili ya wapendwa wetu hapa, kuweni
wastaarabu kwa sababu mbele yetu kuna wana usalama ambao wanalinda amani,
ingawa kufa ni kufa tu, wenzetu wameshakufa na sisi ipo siku tutakufa, lakini
kila anayetangulia lazima tumzike kwa heshima zote.”
Kauli hiyo iliwachefua polisi ambao walishatangaza amri ya
watu kutawanyika katika viwanja hivyo na kwamba hakutakuwa na suala la kuaga
miili ya watu hao katika eneo hilo. Ghasia hizo zilisababisha kusimama kwa
shughuli za biashara na kijamii kwa muda jijini Arusha huku watu waliokuwa katika
nyumba zilizokuwa karibu na maeneo yalikorushwa mabomu wakilazimika kutoka nje
kupata hewa safi baada ya nyumba hizo kujaa hewa ya mabomu.
Polisi waliokuwa wakirusha mabomu waliwakimbiza wananchi
hadi maeneo ya Sakina huku wakiendelea kufyatua mabomu kila walipoona
mkusanyiko wa watu.
Katika eneo la Kaloleni , mkabala na Ofisi ya Mtendaji wa
Kata hiyo baadhi ya wafuasi wa Chadema walichoma matairi barabarani na
kusababisha ifungwe. Pia walichoma matairi katika eneo la Mianzini
Katika eneo la Tanki la Maji , Barabara ya kwenda Moshi,
baadhi ya wafuasi wa Chadema walipanga mawe barabarani na kusababisha
msongamano wa magari.
Katikati ya jijini Arusha barabara zilikuwa hazipitiki
kutokana na nyingine kufungwa na kusababisha usumbufu mkubwa.
Waandishi nao matatani
Katika vurugu hizo, baadhi ya waandishi wa habari
walishambuliwa na polisi. Hao ni pamoja na Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la
The Citizen, Zephania Ubwani ambaye kabla ya kuchomoka katika mikono ya askari,
alikuwa akiwaonyesha kitambulisho chake cha kazi.
Hata hivyo, askari hao walimtishia kumtandika na kisha
kumwambia aondoke katika eneo hilo kwa kuwa haijalishi yeye ni nani.
Mwingine ni mwandishi wa gazeti la Nipashe, Cnythia
Mwilolezi ambaye alilazimika kuacha viatu na vitendea kazi vyake katika Uwanja
wa Soweto na kukimbilia kwenye moja ya nyumba zilizopo jirani na eneo la tukio.
Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa
Arusha, Moses Kilyinga alipigwa na polisi baada ya kuonekana akichukua maelezo.
Kilyinga ambaye alishambuliwa na askari hao alisema mara
baada ya askari hao kumkamata, alijitambulisha lakini hawakumwelewa na
wakaendelea kumchapa kabla ya kufanikiwa kuchomoka.
Polisi wavamia hospitali
Wakati baadhi ya majeruhi wakidai kushuhudia polisi
wakiwapiga risasi watu waliokuwa wakimkimbiza mtu aliyerusha bomu katika tukio
la Jumamosi, askari hao juzi walifika katika Hospitali ya Seliani saa mbili
usiku wakitaka kumchukua mmoja wa majeruhi kwa mahojiano kuhusiana na tukio
hilo. Hata hivyo, hawakufanikiwa baada ya mgonjwa kutokomea kusikojulikana
baada ya kupata taarifa za kutaka kuhusishwa na tukio hilo.
Ingawa si polisi wala Chadema waliokuwa tayari kumtaja
mgonjwa huyo, inaelezwa kwamba majeruhi anayesakwa ni Abdallah Alila
aliyekaririwa na vyombo vya habari jana na juzi akidai kumshuhudia aliyerusha
boma akiondoka kwenye moja ya magari ya polisi.
Hata hivyo, Kamishna Chagonja jana alisema kwamba jeshi lake
linapenda kushirikiana na raia kupata taarifa na si kutumia nguvu katika
kukusanya ushahidi wake.
S.T. T. Mwananchi
EmoticonEmoticon